JINA LA CHAPA

Bio‑Oil®

JINA LA BIDHAA NA UKUBWA

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya 25ml

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya 60ml

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya 125ml

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya 200ml

MAELEZO

Mafuta ya kutunza ngozi yaliyothibitishwa kimatibabu kusaidia kuboresha muonekano wa makovu na alama za kunyoosha ngozi.

DALILI

Makovu

Husaidia kuboresha mwonekano wa makovu mapya na ya zamani.

Michirizi kwenye ngozi

Husaidia kuboresha mwonekano wa michirizi kwenye ngozi. Pia husaidia kuboresha mnyumbuko wa ngozi, na hivyo kupunguza uwezekano wa michirizi kwenye ngozi kutokea.

Rangi ya ngozi isiyo sawia

Husaidia kuboresha mwonekano rangi ya ngozi isiyo sawia.

Kuzeeka kwa ngozi

Husaidia kuboresha mwonekano wa kuzeeka kwa ngozi kwenye uso na mwili.

Ngozi iliyokauka

Husaidia kupunguza upotezaji wa unyevu na huboresha mwonekano wa ngozi iliyokauka.

ONYESHO

Mafuta ya rangi ya machungwa / waridi.

VIUNGO

Paraffinum Liquidum, Triisononanoin, Cetearyl Ethylhexanoate, Isopropili Myristate, Retinyl Palmitate, Mafuta ya Mbegu ya Helianthus Annuus, Tocopheryl Acetate, Mafuta ya Maua ya Anthemis Nobilis, Mafuta ya Lavandula Angustifolia, Mafuta ya Majani ya Rosmarinus Officinalis, Kiziduo cha Calendula Officinalis, Mafuta ya Glycine Soja, Bisabolol, Tocopherol, Manukato, Alpha-Isomethyl Ionone, Amyl Cinnamal, Benzyl Salicylate, Citronellol, Coumarin, Eugenol, Farnesol, Geraniol, Hydroxycitronellal, Limonene, Linalool, CI 26100.

JARIBIO LA KIMATIBABU LA MAKOVU

Kituo cha majaribio

proDERM Institute for Applied Dermatological Research, Hamburg, Germany.

Lengo

Kutathmini ufanisi wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® katika kuboresha mwonekano wa makovu.

Sampuli

Washiriki: Washiriki 36 wa kike wenye aina mbalimbali za ngozi za Fitzpatrick. Umri wa makovu: umbo jipya hadi umri wa miaka 3. Maeneo ya makovu: tumbo, mguu, mkono, shingo, goti, shina, mwili wa juu. Umri wa washiriki: 18–65.

Mbinu

Utafiti fiche, wa nasibu na unaothibitiwa wa kipozauongo. Washiriki walikuwa na makovu yanayolingana au kovu linalotosha kuruhusu matumizi nusu nusu ya kovu na uwezo wa kulinganisha wahusika. Bidhaa ilitumiwa mara mbili kila siku kwa wiki 8; hakuna usingaji wa ziada uliyofanywa kwenye eneo lengwa. matumizi yalifanywa chini ya usimamizi katika vipindi vya mara kwa mara. Tathmini zilifanywa katika wiki ya 0, 2, 4 na 8. Vigezo tofauti vya kovu kama ilivyofafanuliwa katika Mizani ya Tathmini ya Makovu kutoka kwa mtazamo wa Mgonjwa na Daktari (POSAS) vilitathminiwa.

Matokeo

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® ni mazuri katika kuboresha mwonekano wa makovu. Matokeo muhimu ya takwimu yalipatikana baada ya wiki 2 tu (siku ya 15), dhahiri katika asilimia 66% ya wahusika. Baada ya wiki 8 (siku ya 57) asilimia 92% ya wahusika walionekana kupata nafuu, huku kiwango cha kupata nafuu kikiwa karibu mara tatu ya wiki ya 2. Unafuu endelevu wa POSAS katika muda wa utafiti huu.

UTAFITI WA MAKOVU YA CHUNUSI

Kituo cha majaribio

Dept. of Dermatology, Peking University First Hospital, Beijing, China.

Lengo

Utafiti wa kutathmini ufanisi wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® katika kuboresha mwonekano wa makovu ya chunusi kwenye uso wa wahusika Wachina.

Sampuli

Wahusika: Wahusika 44 wa Kichina wenye makovu mapya ya chunusi usoni (<umri wa miaka 1). Washiriki waliotibiwa kwa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® walikuwa wahusika 32 na wahusika wasiotibiwa walikuwa wahusika 12. Umri wa washiriki: 14–30.

Mbinu

Utafiti unaomficha mhusika, unaodhibitiwa na wa nasibu. Wahusika walishiriki katika tathmini ya kwanza ya uchunguzi ikifuatiwa na kipindi cha kuondoa matibabu cha wiki 1. Bidhaa ilitumiwa mara mbili kwa siku kwa wiki 10. matumizi yalifanywa chini ya usimamizi katika vipindi vya mara kwa mara. Tathmini iliyofanywa katika wiki ya 0, 4, 8 na 10 ni pamoja na yafuatayo: Tathmini ya alama ya kimataifa ya makovu (GSS) iliyofanywa na mchunguzi, kipimo cha rangi ya kovu ya chunusi / wekundu kwa kutumia chromameter, kipimo cha viwango vya mafuta ya ngozi kwa kutumia sebumeter, nyaraka za idadi ya mabaka na vidonda zilizoandikwa na mtaalamu wa ngozi. Wahusika pia walikamilisha maswali ya kujitathmini katika kila ziara.

Matokeo

Matokeo bora ya uainishaji wa kimatibabu yalikuwa uwezo wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® kupunguza harara au wekundu wa makovu ya chunusi, huku ngozi kwa ujumla ikingaa zaidi. Matokeo ya dodoso la kujitathmini yalionyesha kuwa zaidi ya asilimia 84% ya wahusika walipata nafuu katika hali ya jumla ya makovu yao ya chunusi na zaidi ya asilimia 90% walipata nafuu katika rangi ya kovu. Hesabu ya chunusi na matokeo ya kipimo cha mafuta ya ngozi yalionyesha kuwa kutumia Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® hakusababishi au kuongeza chunusi au kuongeza utoaji wa mafuta ya ngozi.

JARIBIO LA KIMATIBABU LA MICHIRIZI KWENYE NGOZI

Kituo cha majaribio

proDERM Institute for Applied Dermatological Research, Hamburg, Germany.

Lengo

Kufikia ufanisi wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® katika kuboresha mwonekano wa michirizi kwenye ngozi.

Sampuli

Washiriki: Washiriki 38 wa kike wenye aina mbalimbali za ngozi za Fitzpatrick. Sababu za michirizi kwenye ngozi: mbalimbali (baada ya ujauzito, kuongezeka kwa uzani au ukuaji wa haraka katika miaka ya ujana). Maeneo ya alama ya kunyoosha: tumbo, mapaja na viuno. Umri wa washiriki: 18–65.

Mbinu

Utafiti fiche, wa nasibu na unaothibitiwa wa kipozauongo. Wahusika walikuwa na michirizi inayolingana kwenye ngozi au michirizi kwenye ngozi inayotosha kuruhusu matumizi nusu nusu kwenye michirizi na uwezo wa kulinganisha wahusika. Bidhaa ilitumiwa mara mbili kila siku kwa wiki 8, hakuna usingaji wa ziada uliyofanywa kwenye eneo lengwa. matumizi yalifanywa chini ya usimamizi katika vipindi vya mara kwa mara. Tathmini zilifanywa katika wiki ya 0, 2, 4 na 8. Vigezo tofauti vya kovu kama ilivyofafanuliwa katika Mizani ya Tathmini ya Makovu kutoka kwa mtazamo wa Mgonjwa na Daktari (POSAS) vilitathminiwa.

Matokeo

Kutathmini ufanisi wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® katika kuboresha mwonekano wa michirizi kwenye ngozi. Matokeo muhimu kitakwimu yalipatikana baada ya wiki 2 tu (siku ya 15), yaliyoshuhudiwa katika asilimia 95% ya wahusika. Baada ya wiki 8 (siku ya 57) asilimia 100% ya wahusika walionekana kupata nafuu, huku kiwango cha kupata nafuu kikiwa karibu mara mbili ya wiki ya 2. Unafuu endelevu wa POSAS katika muda wa utafiti huu.

JARIBIO LA KIMATIBABU LA RANGI YA NGOZI ISIYO SAWIA

Kituo cha majaribio

Thomas J. Stephens & Associates, Inc., Texas, United States of America.

Lengo

Kutathmini ufanisi wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® katika kuboresha mwonekano wa rangi ya ngozi isiyo sawia na rangi isiyolingana wakati inatumiwa na wanawake wenye ngozi inayoathiriwa kidogo hadi wastani na mwanga wa jua (kuzeeka) kwenye uso na shingo.

Sampuli

Washiriki: Washiriki 67 wa kike wenye aina mbalimbali za ngozi za Fitzpatrick waliobainishwa kimatibabu kuathiriwa kidogo hadi wastani na mwanga wa jua kwenye uso na shingo. Washiriki waliotibiwa kwa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® walikuwa wahusika 35 na washiriki wasiotibiwa walikuwa wahusika 32. Umri wa washiriki: 30–70.

Mbinu

Utafiti unaomficha mhusika, unaodhibitiwa na wa nasibu. Wahusika walishiriki katika tathmini ya kwanza ya uchunguzi ikifuatiwa na kipindi cha kuondoa matibabu cha wiki 1. Bidhaa ilitumiwa kwenye uso na shingo mara mbili kila siku kwa wiki 12. Matumizi yalifanywa chini ya usimamizi katika ziara rasmi ya kwanza. Tathmini za kimatibabu zilizofanywa katika wiki ya 0, 2, 4, 8 na 12. Wahusika walipewa alama tofauti za kimatibabu kwenye uso na shingo ili kuangalia rangi ya ngozi isiyo sawia na rangi isiyolingana.

Matokeo

Ufanisi wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® katika kuboresha mwonekano wa rangi ya ngozi isiyo sawia na rangi isiyolingana katika ngozi inayoathiriwa na mwangaza jua (kuzeeka). Baada ya wiki 4 matokeo muhimu kitakwimu yalipatikana katika vigezo vyote kwenye uso na shingo. Baada ya wiki 12, asilimia 86% ya wahusika (wanawake) wanaotibiwa kwa kutumia Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® walionyesha kuimarika pakubwa kitakwimu katika rangi ya ngozi isiyo sawia kwenye uso, asilimia 71% ya wahusika (wanawake) katika rangi isiyolingana kwenye uso, asilimia 69% katika rangi ya ngozi isiyo sawia kwenye shingo na asilimia 60% katika rangi isiyolingana kwenye shingo.

JARIBIO LA KIMATIBABU LA KUZEEKA KWA NGOZI

Kituo cha majaribio

Thomas J. Stephens & Associates, Inc., Texas, United States of America.

Utafiti wa 1: Uso na shingo

Lengo

Kutathmini ufanisi wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® ikitumiwa na wanawake wenye ngozi inayoathiriwa kidogo hadi wastani na mwanga wa jua (kuzeeka) kwenye uso na shingo.

Sampuli

Washiriki: Washiriki 67 wa kike wenye aina mbalimbali za ngozi za Fitzpatrick waliobainishwa kimatibabu kuathiriwa kidogo hadi wastani na mwanga wa jua kwenye uso na shingo. Washiriki waliotibiwa kwa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® walikuwa wahusika 35 na washiriki wasiotibiwa walikuwa wahusika 32. Umri wa washiriki: 30–70.

Mbinu

Utafiti unaomficha mhusika, unaodhibitiwa na wa nasibu. Wahusika walishiriki katika tathmini ya kwanza ya uchunguzi ikifuatiwa na kipindi cha kuondoa matibabu cha wiki 1. Bidhaa ilitumiwa kwenye uso na shingo mara mbili kila siku kwa wiki 12. Matumizi yalifanywa chini ya usimamizi katika ziara rasmi ya kwanza. Tathmini za kimatibabu zilifanywa katika wiki ya 0, 2, 4, 8 na 12. Wahusika walipewa alama tofauti za kimatibabu kwenye uso na shingo kwa vigezo vifuatavyo vya ufanisi: mwonekano wa jumla, mistari laini, makunyanzi makubwa, rangi isiyolingana, rangi ya ngozi isiyo sawia, mwonekano wa kuparara / ulaini, hisia ya kuparara / ulaini, mwonekano thabiti, na wangavu (kutong’aa).

Matokeo

Ufanisi wa Mafuta ya Kutunza Ngozi Bio‑Oil® katika kuboresha mwonekano wa jumla katika ngozi inayoathiriwa na mwangaza jua (kuzeeka) kwenye uso na shingo. Baada ya wiki 8 matokeo muhimu kitakwimu yalipatikana katika vigezo vyote vya vya ufanisi vilivyopewa alama za kimatibabu. Baada ya wiki 12 asilimia 94% ya wahusika waliotibiwa kwa kutumia Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® walionyesha kuimarika pakubwa kitakwimu katika mwonekano wa jumla kwenye uso na asilimia 80% ya wahusika walionyesha kuimarika pakubwa kitakwimu katika mwonekano wa jumla kwenye shingo.

Utafiti wa 2: Mwili

Lengo

Kutathmini ufanisi wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® ikitumiwa kwenye ngozi ya sehemu ya juu ya kichwa, mguu wa chini na mkono na wanawake wenye ngozi inayoathiriwa kidogo hadi wastani na mwanga wa jua (kuzeeka).

Sampuli

Washiriki: Washiriki 67 wa kike wenye aina mbalimbali za ngozi za Fitzpatrick waliobainishwa kimatibabu kuathiriwa kidogo hadi wastani na mwanga wa jua kwenye uso na shingo. Washiriki waliotibiwa kwa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® walikuwa wahusika 35 na washiriki wasiotibiwa walikuwa wahusika 32. Umri wa washiriki: 30–70.

Mbinu

Utafiti unaomficha mhusika, unaodhibitiwa na wa nasibu. Wahusika walishiriki katika tathmini ya kwanza ya uchunguzi ikifuatiwa na kipindi cha kuondoa matibabu cha wiki 1. Bidhaa ilitumiwa kwenye kwa sehemu ya juu ya kichwa, miguu ya chini na mikono mara mbili kila siku kwa wiki 12. Matumizi yalifanywa chini ya usimamizi katika ziara rasmi ya kwanza. Tathmini za kimatibabu zilifanywa katika wiki ya 0, 2, 4, 8 na 12. Wahusika (wanawake) walipewa alama tofauti za kimatibabu za sehemu ya juu ya kichwa, miguu ya chini na mikono kulingana na vigezo vifuatavyo vya ufanisi: mwonekano wa jumla, makunyanzi makubwa, ukavu / magamba, mwonekano wa kuparara / ulaini, na hisia ya kuparara / ulaini.

Matokeo

Ufanisi wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® katika kuboresha mwonekano wa jumla katika ngozi inayoathiriwa na mwangaza jua (kuzeeka) kwenye mwili. Baada ya wiki 4 matokeo muhimu kitakwimu yalipatikana katika vigezo vyote vya vya ufanisi vilivyopewa alama za kimatibabu. Baada ya wiki 12 asilimia 89% ya wahusika waliotibiwa kwa kutumia Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® walionyesha kuimarika pakubwa kitakwimu katika mwonekano wa jumla wa sehemu ya juu ya kichwa, miguu ya chini na mikono.

JARIBIO LA KIMATIBABU LA NGOZI ILIYOKAUKA

Kituo cha majaribio

Photobiology Laboratory of the Medical University of South Africa.

Utafiti wa 1: Unyevu wa ngozi ya juu zaidi na kazi ya kuzuia

Lengo

Kutathmini athari za kutumia mara moja Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® ili kuboresha kazi ya unyevu na kuzuia ngozi ya juu zaidi (SC).

Sampuli

Washiriki: Washiriki 40 wa kike wenye aina mbalimbali za ngozi za Fitzpatrick. Eneo la jaribio:bidhaa zinazojaribiwa zilitumiwa kwenye mkono wa mbele wa wahusika wote. Umri wa washiriki: 25–65.

Mbinu

Tathmini ya unyevu wa ngozi kwa kutumia Corneometer kama kipimo msingi, tathmini ya kazi ya kuzuia kwa kutumia Vapometer kama kipimo cha pili. Washiriki waliosha vigasha vyao kwa sabuni saa 2 kabla ya vipimo kuchukuliwa ili kusababisha ukavu wa ngozi. Vipimo msingi vya kifani vilichukuliwa. Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® na mafuta ya ukadiriaji yalitumiwa kwenye maeneo tofauti ya mkono wa mbele wa wahusika wote. Vipimo vilichukuliwa tena mara moja baada ya matumizi ya bidhaa na saa 2 baadaye, kabla na baada ya kuondoa bidhaa. Eneo lisilotibiwa lilipimwa pia nyakati zote.

Matokeo

Baada ya matumizi ya papo hapo, mafuta yote yalipunguza maji yanayotoka kwenye ngozi (TEWL) ikilinganishwa na wale wasiotibiwa. Thamani iliyoongezeka ya uwezo wa ngozi katika muda wa saa 2 kabla ya kuondoa bidhaa ilionyesha kuongezeka kwa unyevu wa ngozi kwa mafuta yote mawili. Saa mbili baadaye, baada ya kuondoa mafuta kwenye uso, Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yalionyesha ongezeko zaidi la thamani za TEWL ikilinganishwa na mafuta ya ukadiriaji, hivyo kuonyesha kuongezeka kwa unyevu na kwa hivyo kuongezeka kwa uyenvu wa ngozi.

Utafiti wa 2: Mwonekano wa ngozi kavu.

Lengo

Kutathmini athari za matumizi ya mara mbili ya kila siku ya Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® kwa ajili ya utendaji wa ulainishaji na utulizaji wa ngozi kavu.

Sampuli

Washiriki: Washiriki 25 walioonyesha kimatibabu kuwa na ngozi kavu / kavu sana katika sehemu ya nje ya miguu ya chini. Eneo la jaribio: bidhaa inayojaribiwa ilitumiwa kwenye sehemu ya nje ya mguu wa chini ya wahusika wote. Umri wa washiriki: 25–65.

Mbinu

Sabuni ilitumiwa ili kufanya ngozi kuwa kavu kwa kipindi cha siku 7. Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® na mafuta ya ukadiriaji yalitumiwa mara mbili kila siku. Uchunguzi wa ngozi ulifanywa siku ya 1 na 3. Tathmini za kuangalia zilifanywa na mtathmini mtaalamu wa kuangalia kwa kutumia taa ya kukuza 2x. Eneo lisilotibiwa lilitathminiwa pia nyakati zote.

Matokeo

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® na mafuta ya ukadiriaji yaliboresha ukavu wa ngozi ikilinganishwa na wahusika wasiotibiwa. Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yalikuwa bora zaidi kitakwimu katika siku ya 3. Maboresho makubwa katika mwonekano wa kuona wa maeneo ya ngozi yaliyotibiwa na kwa kutumia Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yalithibitisha ufanisi wake katika kupunguza ngozi kavu.

Matokeo ya Utafiti wa Pamoja

Kuimarika pakubwa katika mwonekano wa ngozi kavu iliyotibiwa kwa kutumia Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® katika utafiti wa 2 kunathibitisha ufanisi wake katika kutuliza ngozi iliyokauka. Hii inaungwa mkono zaidi na maboresho katika kazi ya kuzuia ya ngozi ya juu zaidi na uwezo wa ngozi katika tafiti zote mbili.

JARIBIO KWENYE NGOZI INAYOATHIRIKA KWA URAHISI

Kituo cha majaribio

Complife Italia S.r.l, Italia.

Lengo

Kutathmini uwezo wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® kusababisha mwasho wa ngozi.

Sampuli

Wahusika: Washiriki 25; 19 wa kike na 6 wa kiume, wote wakiwa na ngozi inayoathirika kwa urahisi kulingana na jaribio la kuathiriwa na asidi ya maziwa. Umri wa washiriki: 18–70.

Mbinu

Utafiti wa nasibu na unaodhibitiwa. Maeneo mawili yalitathminiwa: eneo ambalo udhibiti hasi ulitumika (maji yaliyosafishwa) na eneo ambalo Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® ilitumika. Bidhaa zinazojaribiwa zilitumiwa nyuma ya mikono ya washiriki kwa kipindi cha saa 48 kwa kutumia Finn Chamber®. Matokeo ya ngozi yalitathminiwa chini ya usimamizi wa daktari wa ngozi, ili kutathmini mwasho wa kwanza wa ngozi kwa dakika 15, saa 1 na saa 24 baada ya kuondolewa kwa pamba. Matokeo ya ngozi yalikadiriwa kwenye mizani inayoanzia 0–4 (huku 0 ikiwa hakuna harara, uvimbe, au aina nyingine za mwasho wa ngozi, na 4 ikiwa harara na uvimbe mkali, inayoashiria mwonekano wa rangi nyekundu iliyokolea na uvimbe ulioenea zaidi ya eneo lililotumika).

Matokeo

Uwezo wa ngozi kustahimili wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® ulichukuliwa kuwa 'usiowasha'.

JARIBIO LA KUTOSABABISHA CHUNUSI

Kituo cha majaribio

Complife Italia S.r.l, Italia.

Lengo

Ili kujaribu ikiwa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yanaweza kusababisha chunusi na mabaka (chunusi).

Sampuli

Wahusika: Washiriki 20; 14 wa kike na 6 wa kiume wenye aina tofauti za ngozi ya Fitzpatrick na wanaoweza kuathiriwa na chunusi. Umri wa washiriki: 18–65.

Mbinu

Utafiti wa nasibu na unaodhibitiwa. Bidhaa hiyo ilitumiwa kwenye karatasi ya ufyonzaji na kupakwa kwenye eneo la juu la migongo ya washiriki. Pamba hizo ziliachwa kwa saa 48 hadi 72, zikaondolewa na kutumiwa tena. Jumla ya pamba 12 zilitumika kwa wiki 4 mfululizo. Maeneo matatu yalitathminiwa kwa kulinganisha udhibiti hasi (maji yaliyosafishwa), bidhaa inayojaribiwa (Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil®) na udhibiti chanya (kileo cha lanolini, bidhaa inayojulikana kusababisha chunusi). Matokeo ya ngozi yatathminiwa chini ya usimamizi wa daktari wa ngozi dakika 15 baada ya kuondolewa kwa kila pamba ili kulinganisha uwepo wa mabaka kabla na baada ya kutumiwa kwa kila bidhaa.

Matokeo

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yalipatikana kuwa hayasababishi chunusi. Eneo ambalo Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® ilitumika halikuonyesha tofauti kubwa ikilinganishwa na eneo la udhibiti hasi. Udhibiti chanya ulisababisha chunusi.

UTAFITI WA UFYONZAJI

Kituo cha majaribio

proDERM Institute for Applied Dermatological Research, Hamburg, Germany.

Utafiti wa 1: Wakadiriaji wataalamu

Lengo

Kutathmini kiwango cha ufyonzaji wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® baada ya matumizi ya kawaida na kusugua.

Sampuli

Wahusika: Wakadiriaji 22 wataalamu; 21 wa kike na 1 wa kiume. Eneo la jaribio: bidhaa zinazojaribiwa zilitumiwa kwenye mkono wa mbele wa wakadiriaji wote. Umri wa washiriki: 18–70.

Mbinu

Utafiti fiche, wa nasibu na unaothibitiwa. Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® na mafuta ya ukadiriaji yalitumiwa kwenye maeneo yaliyoteuliwa ya mkono wa mbele wa wakadiriaji wote. Wakadiriaji walitekeleza mienendo 100 ya kuendesha baisikeli kwa kasi iliyobainishwa. Kisha wakadiriaji walikadiria ufyonzaji wa bidhaa kwenye mizani ya alama 5 kuanzia 'inafyonza polepole sana' hadi 'inafyonza haraka sana'. Vipimo vya Sebumeter, vya kutathmini kiasi cha mafuta kwenye ngozi, vilichukuliwa mara mbili kwa wakati tofauti; Kabla ya kutumia na dakika 2 baada ya kutumia bidhaa.

Matokeo

Ufyonzaji wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® kwenye ngozi ulitathminiwa kuwa 'wa haraka sana' au 'wa haraka' na wengi (asilimia 77.3%) ya wakadiriaji wataalamu. Hii ilithibitishwa kupitia kipimo kifani kwa kutumia usomaji wa sebumeter wakati wa pili ambao ulionyesha kuwa kiasi cha Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® kilichobaki kwenye ngozi kilikuwa chini sana ikilinganishwa na mafuta ya ukadiriaji.

Utafiti wa 2: Jopo la watumiaji

Lengo

Kutathmini kiwango cha ufyonzaji wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® baada ya matumizi ya kawaida na kusugua.

Sampuli

Wahusika: Washiriki 100; 97 wa kike na 3 wa kiume. Eneo la jaribio: bidhaa zinazojaribiwa zilitumiwa kwenye mkono wa mbele wa washiriki wote. Umri wa washiriki: 18–70.

Mbinu

Utafiti fiche, wa nasibu na unaothibitiwa. Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® na mafuta ya ukadiriaji yalitumiwa kwenye maeneo yaliyoteuliwa ya mkono wa mbele wa washiriki wote. Washiriki walisugua bidhaa inayojaribiwa kwa dakika moja kila mmoja. Kisha washiriki walikadiria ufyonzaji wa bidhaa kwenye mizani ya alama 5 kuanzia 'inafyonza polepole sana' hadi 'inafyonza haraka sana'.

Matokeo

Ufyonzaji wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® kwenye ngozi ulitathminiwa kuwa 'wa haraka sana' au 'wa haraka' na wengi (asilimia 72%) ya washiriki.

UTAFITI WA UWEZO WA KUZIBA

Kituo cha majaribio

Kesi iliyoendeshwa na Profesa Dkt. J Wiechers katika Maabara ya Rigano, Milan, Italia.

Lengo

Kutathmini kama Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yanaonyesha kiwango sawa cha kuziba kama utando unaolinda ngozi ya kijusi. Utando unaolinda ngozi ya kijusi unazingatiwa sana na wanasayansi wa vipodozi kama 'kipimo bora zaidi' katika ulainishaji wa ngozi kwa sababu ya kiwango chake bora cha kuziba.

Mbinu

Kiasi kinachojulikana cha maji kiliwekwa katika bika kikiwa kimefunikwa kwa utando unaoweza kupenyeza nusu uitwao Vitro-Skin, ambao unaiga sifa za sehemu ya juu ya ngozi ya binadamu. Kiasi sawa cha utando unaolinda ngozi ya kijusi na Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® kilitumiwa kwenye utando na kiwango cha kupoteza maji kutoka kwenye bika kilipimwa over time. Hii ililinganishwa na kiwango cha kupoteza maji bila bidhaa yoyote kwenye utando. Kiwango cha uhamishaji wa mvuke wa maji kwa kila bidhaa kilihesabiwa na kuonyeshwa katika g / m² / h.

Matokeo

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yalionyesha kiwango sawa cha kuzia kama utando unaolinda ngozi ya kijusi, iliandikisha 23.5 ikilinganishwa na 27.2 ya utando unaolinda ngozi ya kijusi.

MATUMIZI

Jinsi ya kutumia

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yanapaswa kusingwa kwa mwendo wa mviringo kwenye mwili hadi ifyonzwe kabisa. Inashauriwa kwamba bidhaa hiyo itumiwe mara mbili kwa siku, kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu. Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® hayapaswi kutumiwa kwenye kidonda wazi au ngozi iliyokatika. Imekusudiwa kutumiwa kama kipodozi tu. Ni salama kutumia kwenye kovu mara tu ngozi iliyo juu imepona kabisa. Matokeo yatatofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Epuka isiingie machoni. Ikiwa itaingia machoni, safisha macho vizuri kwa maji safi. Usiweke karibu na watoto.

Muda wa kutumia

Jaribio la kimatibabu la Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® limefanywa kwa kipindi cha wiki 8 na wiki 12, hivyo kuruhusu utendaji wa bidhaa hiyo kutathminiwa baada ya muda. Uchambuzi wa takwimu unaonyesha uboreshaji mkubwa katika mwonekano wa ngozi baada ya muda mfupi kama wiki mbili na kwamba uboreshaji huu unadumishwa au huongezeka kwa muda wa majaribio yote. Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® hata hivyo yanaweza kutumika kila wakati.

Tumia pamoja na utaratibu wa utunzaji wa ngozi

Kwa ufyonzaji wa juu, Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yanapaswa kutumiwa kwenye ngozi iliyosafishwa. Kuchanganya Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® na bidhaa nyingine ili 'kuifanya ifanye kazi zaidi' kunaweza kuathiri ufanisi wake. Ikiwa unatumia kilainisha ngozi, losheni ya kukinga jua au krimu nyingine, fanya hivyo tu baada ya Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® kufyonzwa kabisa kwenye ngozi. Kwa matumizi kwenye mwili mzima, tumia Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® baada ya kuoga.

Kutumia wakati wa ujauzito

Michirizi kwenye ngozi wakati wa ujauzito inaweza kuonekana mahali popote kwenye mwili, lakini ina uwezekano mkubwa wa kuonekana kwenye fumbatio, mapaja, nyonga, mgongo wa chini, makalio na matiti. Ili kusaidia kuzuia utokeaji wa michirizi kwenye ngozi wakati wa ujauzito, inashauriwa kwamba Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yatumike kwenye maeneo haya mara mbili kwa siku, tangu kuanza kwa miezi mitatu ya kwanza hadi baada ya kujifungua. Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yakitumiwa mara kwa mara itatoa pia utulivu wa ngozi inayowasha na iliyokauka, inayohusishwa na mwasho mkali wa ujauzito. Inaweza pia kutumika kwenye rangi ya ngozi isiyo sawia ambayo hutokana na kubadilika kwa homoni ambayo hutokea wakati wa ujauzito.

Vitamini A na ujauzito

Wanawake kwa kawaida wanapendekezewa kupunguza virutubisho vya vitamini A wakati wa ujauzito na kwa hivyo wanaweza kuwa na wasiwasi kuhusu kutumia bidhaa za ngozi zenye vitamini A. Dutu yoyote inayotumika kwenye ngozi ni hatari tu ikiwa iko katika viwango vya juu kuliko kiwango chake cha juu cha sumu. Kwa sababu ngozi hutoa kizuizi kikubwa cha upenyaji, sehemu ndogo tu ya vitamini A inayotumiwa ndio huingia mwilini. Kamati ya Sayansi ya Tume ya Ulaya kuhusu Usalama wa Watumiaji (SCCS) imetathmini vitamini A na michanganyiko yake, inapotumiwa kama viungo vya vipodozi. Maoni ya SCCS ni kwamba matumizi ya vitamini A katika losheni za mwili, hadi kiwango cha juu zaidi cha asilimia 0.05% ya retinoli, ni salama. Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yana vitamini A katika muundo wake iliyo chini ya kiwango hiki cha juu zaidi kinachoruhusiwa kwa losheni ya mwili na inaweza kutumika kwa usalama wakati wa ujauzito. Kwa kujumuisha vitamini A kwa kiwango cha chini, Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® huwapa wanawake wajawazito faida za vitamini A bila hatari yoyote ya usalama.

Mafuta ya Rosemary na ujauzito

Mafuta ya Rosemary katika viwango vya juu yameonekana kuwa na uwezo wa kuongeza mtiririko wa damu, kumaanisha kuwa yana uwezo wa kuchochea hedhi na uwezekano wa kusababisha uchungu wa uzazi wa mapema. Hii ndio sababu wataalamu wa tiba mimea na mitishamba wanaotumia mafuta ya rosemary katika viwango vya juu, wanapendekeza kutoyatumia wakati wa ujauzito. Hata hivyo, kiwango cha mafuta ya rosemary katika Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® ni cha chini sana na kwa hivyo ni salama kutumia wakati wa ujauzito.

Kutumia wakati wa kunyonyesha

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® ni salama kutumiwa kwenye mwili wakati wa kunyonyesha, lakini inapendekezwa kuepuka kutumia kwenye chuchu. Ingawa hakuna madhara yanayoweza kutokea, watoto wachanga wanaweza kuathiriwa kwa urahisi na hawapaswi kumeza Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil®, hata kwa kiasi kidogo sana.

Matumizi kwa watoto wachanga na wakubwa

Usalama wa kutumia Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® kwa watoto chini ya umri wa miaka mitatu haujatathminiwa. Katika miaka michache ya kwanza baada ya kuzaliwa, mabadiliko mengi hufanyika katika mwili wa binadamu, ikiwa ni pamoja na kukua kwa mfumo wa kinga. Kwa hivyo inashauriwa kwamba itumiwe tu kwa watoto wenye umri wa miaka mitatu au zaidi. Bidhaa hii inapaswa kutumiwa kwa uangalifu kwa watoto na haipaswi kutumiwa karibu na macho au mdomo.

Kutumia kwenye jua

Majaribio yaliyofanywa kwenye Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yalionyesha kuwa bidhaa hii haiwezeshi au kuzidisha kuchomwa na jua. Kwa hivyo ni salama kutumia kukiwa na jua, hata hivyo bidhaa hii haitoi kinga dhidi ya madhara ya mionzi ya jua ya UVA na UVB na hivyo ni muhimu kutumia bidhaa hii pamoja na bidhaa nyingine za kukinga mionzi ya jua zenye sifa ya kukinga jua (SPF) ya angalau 30.

Kutumia kwenye au karibu na tando telezi

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yameainishwa kuwa salama kwa matumizi yote, isipokuwa kwenye tando telezi.

Kutumia pamoja na tibaredio au tibakemikali

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® ni bidhaa ya vipodozi. Inashauriwa kwa watu wanaofanyiwa matibabu ya tiba ya mionzi au tiba ya kemikali kutafuta ushauri wa daktari kabla ya kutumia bidhaa hiyo.

Kutumia pamoja na bidhaa za dawa

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® ni bidhaa ya vipodozi. Kwa ushauri kuhusu kutumia bidhaa hii pamoja na kutumia bidhaa za dawa kwa wakati mmoja, ni bora kutafuta ushauri wa daktari.

Kutumia kwenye ngozi inayoathirika kwa urahisi

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yanaweza kutumika kwenye ngozi inayoathirika kwa urahisi. Katika utafiti wa mwasho wa ngozi uliofanyiwa washiriki 25 wenye umri wa miaka 18–65 walio na ngozi inayoathirika kwa urahisi, hakuna wahusika waliopata madhara yoyote mabaya kutokana na muundo huu.

Kuumia kwenye ngozi yenye mafuta

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yanaweza kutumika kwenye ngozi yenye mafuta. Katika jaribio lililofanyiwa washiriki 20 wenye umri wa miaka 18–65 wenye ngozi inayoathiriwa na chunusi, Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yalipatikana kuwa haisababishi chunusi.

Kutumia kwenye ngozi inayoathiriwa na chunusi

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yanaweza kutumika kwenye ngozi inayoathiriwa na chunusi. Katika jaribio lililofanyiwa washiriki 20 wenye umri wa miaka 18–65 wenye ngozi inayoathiriwa na chunusi, Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yalipatikana kuwa haisababishi chunusi. Katika utafiti wa makovu ya chunusi uliofanyiwa wahusika 44 wenye umri wa miaka 14–30 walio na makovu mapya ya chunusi kwenye uso; hesabu ya chunusi na matokeo ya kipimo cha mafuta ya ngozi yalionyesha kuwa kutumia Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® hakusababishi au kuongeza chunusi au kuongeza utoaji wa mafuta ya ngozi. Hata hivyo inashauriwa kwa watu wanaosumbuliwa na chunusi kutafuta ushauri wa daktari kabla ya kutumia Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil®.

KUTOKEA KWA MAKOVU

Kovu ni ukuaji wa kolajeni ambao hutokea kama sehemu ya kawaida ya mchakato wa kupona kufuatia jeraha kwenye ngozi. Kolajeni imeundwa kwa protini za kawaida ambazo huunda sehemu kuu ya tishu unganishi za mwili. Wakati jeraha kwenye ngozi linatokea, mwili hufanya kazi haraka iwezekanavyo kurekebisha eneo lililoathiriwa, kwa kuzingatia kuishi badala ya uponyaji kamili. Uzalishaji huo wa haraka wa kolajeni ili kukabiliana na jeraha ndio huunda makovu. Ijapokuwa kovu litapitia mabadiliko mengi kadri linavyokomaa, halitawahi kupata nguvu ya kawaida ya ngozi inayoizunguka. Vinyweleo na tezi jasho katika eneo la kovu hazitarudi tena. Kutokea kwa makovu kuna awamu nne zifuatazo:

Awamu ya kuzuia damu

Hii huanza mara tu baada ya jeraha kutokea na hudumu kwa saa chache, huku eneo lililojeruhiwa likijaribu kurejesha hali yake ya kawaida kwa kuzuia mishipa ya damu ili kudhibiti damu. Chembe zilizojeruhiwa wakati huo mmoja hutoa protini fulani ili kuwezesha kuganda, hivyo kuziba mishipa iliyoharibiwa na kupunguza upotezaji wa damu.

Awamu ya uvimbe

Wekundu na uvimbe ambao unatokea kwa kipindi cha siku tatu au nne baada ya kiwewe cha kwanza ni kiashiria kinachoonekana cha mfumo wa kinga. Chembe nyeupe za damu hutoa kemikali zinazosafisha jeraha ili kutoa uchafu na bakteria.

Awamu ya kukua kwa haraka

Hii huanza siku ya tatu na huendelea kwa karibu wiki tatu. Michakato mitatu tofauti hutokea kwa wakati mmoja katika awamu hii ili kufunga kidonda: Tishu unganishi: Chembe za fibroblasts (chembe zinazohusika katika kuchanganya kolajeni) huongezeka kwenye eneo la jeraha ili kuunda kolajeni kwa haraka ili kujaza jeraha. Mchakato wa kuziba: safu ya ngozi imeundwa kufunika jeraha. Mpunguo wa jeraha: jeraha huvutwa pamoja katika jaribio la kupunguza kasoro.

Awamu ya kukomaa

Awamu hii ya 'kurekebisha' huanza baada ya takriban wiki tatu na inaweza kuendelea hadi miaka miwili kulingana na ukubwa na kina cha jeraha. Wakati huu, kolajeni huendelea kukua huku nyuzi zikipangwa upya kulingana na mikazo iliyowekwa kwenye eneo la jeraha, hivyo kuamua hali ya mwisho ya kovu. Huku kovu likifunika na kulinda eneo la jeraha, linaweza kuvurugwa kwa urahisi. Kwa ujumla tishu ya kovu huonyesha asilimia 70% ya nguvu ya mkazo wa ngozi ya kawaida.

AINA ZA MAKOVU

Kwa sababu watu hupona kitofauti, mwonekano wa mwisho wa kovu utatofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Mambo kama aina ya ngozi, eneo la kovu, aina ya jeraha, umri wa mtu na hata hali ya lishe itakuwa muhimu katika kuamua kovu litaonekana aje. Aina za makovu zinaweza kugawanywa katika makundi yafuatayo:

Makovu ya kawaida

Makovu haya yanaonekana yamevimba na meusi mwanzoni lakini yanalainika na kutoonekana sana baada ya muda ambayo husababisha kovu lenye mstari mwembamba.

Makovu yaliyodumaa

Makovu haya husababisha mibonyeo au mapengo chini ya ngozi. Mifano ni makovu yanayotokana na chunusi au tetekuwanga.

Makovu yaliyoinuka

Makovu haya huinuka juu ya ngozi. Sifa za makovu haya ni viwango vikubwa vya kolajeni, lakini husalia sikuzote ndani ya mipaka ya jeraha asili.

Makovu mabonge

Makovu mabonge yanapaswa kutofauitishwa na makovu yaliyoinuka. Ingawa pia ni makovu yaliyoinuka, sifa za makovu mabonge ni kwamba yameenea zaidi ya mipaka ya jeraha asili. Yanaweza kuendelea kukua baada ya muda na kawaida hujirudia baada ya mabonge hayo kuondolewa.

Makovu ya mikazo

Kovu la mikazo hutokea wakati ngozi inakaza kabisa. Mara nyingi hutokea wakati makovu yanavuka viungo, au ngozi kukunjana, kwenye pembe za kulia. Tishu ya kovu hili hukataa kunyooka na inaweza kuzuia mienendo ya kawaida. Mara nyingi makovu ya mikazo hutokea baada ya majeraha ya moto.

Michirizi kwenye ngozi (Striae)

Michirizi kwenye ngozi hutokea wakati wa vipindi vya mabadiliko ya haraka katika uzani (kwa mfano ukuaji wa haraka katika miaka ya ujana, ujauzito) wakati mwili unapanuka haraka kuliko ngozi inayoifunika, na kusababisha mipasuko ya ndani katika tishu za ngozi. Wakati mipasuko hii inajirekebisha yenyewe huunda makovu ambayo yanajulikana kama michirizi kwenye ngozi.

UUNDAJI WA MICHIRIZI KWENYE NGOZI

Kwa maneno ya kimatibabu michirizi kwenye ngozi, au striae, ni aina nyingine tu za makovu, hata hivyo, watu wengi huyaona kuwa tofauti na makovu. Striae ni mistari kwenye ngozi ambayo inakua katika vipindi vya upanuzi wa haraka wa ngozi, kwa mfano katika wanawake wajawazito, wajenzi wa mwili, na vijana wakati wa ukuaji wao wa haraka. Inasababishwa na kile ambacho jina like linapendekeza, kunyooka. Watu wenye ngozi nyeupe huwa na michirizi ya ngozi ya rangi ya waridi, huku watu wenye ngozi nyeusi huwa na michirizi ya ngozi ambayo ni nyeupe zaidi ya ngozi inayoizunguka. Kwa kawaida ngozi huwa nyumbufu. Unyumbufu huu hutolewa na kolajeni na elastini kwenye ngozi, ambazo ziko chini ya tishu ya ngozi. Kolajeni imeundwa na kundi la protini za kawaida na ni sehemu kuu ya tishu unganishi za mwili. Elastini, ambayo pia imeundwa kwa protini za kawaida, hupatikana pia katika tishu unganishi na hutoa sifa zake za unyumbufu. Tishu hii unganishi huwezesha ngozi kukabiliana na mwenendo endelevu wa mwili kwa kupanua na kubana, lakini wakati wa vipindi vya kuongeza uzani kwa haraka, inaweza kuwa haina muda wa kutosha wa kurekebisha, hivyo kusababisha mipasuko ya ndani katika tishu ya ngozi. Wakati mipasuko hii inajirekebisha yenyewe inaunda makovu ambayo tunayajua kama michirizi kwenye ngozi. Mfano muhimu ni ule wa springi ikinyooshwa. Ukinyoosha springi kwa kiwango fulani, kinachojulikana kama kikomo chake cha kawaida cha unyumbufu, inarudi kwenye ukubwa wake ya kawaida mara kwa mara. Hata hivyo, ikiwa utanyoosha springi zaidi ya kikomo chake cha kawaida cha unyumbufu, itakuwa imenyooshwa kabisa na haitarudi kwenye ukubwa wake wa kawaida. Ingawa michirizi kwenye mwili haiwakilishi shida kubwa ya kimatibabu, inaweza kusababisha shida ya kihisia kwa wale wanaoipata. Uwezekano wa kuipata hutofautiana kulingana na aina ya ngozi, umri, urithi, lishe na unyevu wa ngozi. Hatua za uundaji wa michirizi kwenye ngozi ni kama zifuatavyo:

Hatua ya kwanza

Michirizi ya mapema kwenye ngozi huonekana kuwa yenye rangi iliyofifia na pia inaweza kuwa inawasha. Ngozi iliyo karibu na michirizi hiyo pia inaweza kuonekana 'imenyooka' na 'nyembamba'.

Hatua ya pili

Polepole michirizi kwenye ngozi itapanuka kwa urefu na upana na kuwa nyeusi na kuonekana zaidi.

Hatua ya tatu

Mara tu michirizi kwenye ngozi inapokomaa na ngozi haivutani tena, itaanza kufifia na kuwa na rangi hafifu zaidi. Inaweza pia kuonekana kuwa na mibonyeo na isiyo na umbo au urefu wa kawaida.

UUNDAJI WA MICHIRIZI KWENYE NGOZI WAKATI WA UJAUZITO

Inakadiriwa kuwa kati ya asilimia 50% na 90% ya wanawake wajawazito wana uwezekano wa kupata michirizi kwenye ngozi. Michirizi kwenye mwili inaweza kukua kwenye fumbatio, mapaja, nyonga, mgongo wa chini, makalio na matiti – maeneo ambayo ngozi hunyooka zaidi mwili ukibadilika wakati wa ujauzito. Ijapokuwa inaweza kuonekana mahali popote kwenye mwili, ina uwezekano mkubwa wa kuonekana katika maeneo ambayo kiasi kikubwa cha mafuta huhifadhiwa. Ijapokuwa michirizi kwenye ngozi huanza kuonekana kwa kawaida wakati wa miezi mitatu ya baadaye ya ujauzito (karibu mwezi wa sita au wa saba) baadhi ya wanawake huanza kuona michirizi kwenye ngozi ikitokea katika miezi mitatu ya kwanza. Michirizi kwenye ngozi wakati wa ujauzito pia inaweza kutokana na maandalizi ya mlango wa kizazi kwa sababu ya ongezeko la homoni. Homoni hizi huvutia maji zaidi kwenye ngozi, ambayo hutuliza mishikamano kati ya nyuzi za kolajeni. Hii inafanya iwe rahisi kwa ngozi kupasuka wakati imenyooshwa na kwa michirizi kwenye ngozi kutokea. Uwezekano wa kupata michirizi kwenye ngozi hutofautiana kulingana na aina ya ngozi, umri, urithi, lishe na unyevu wa ngozi.

TATHMINI YA USALAMA

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yamefanyiwa tathmini ya usalama na mtaalamu wa sumu aliyehitimu na imeainishwa kuwa salama kwa matumizi yake yaliyokusudiwa na watu wazima, ikiwa ni pamoja na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, na watoto zaidi ya umri wa miaka mitatu.

MADHARA MABAYA

Ijapokuwa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yana maelezo salama yanayohusu sumu na inakidhi kanuni za kimataifa kuhusu suala hili, kama ilivyo katika bidhaa zote za vipodozi, kuna hatari kwamba watumiaji wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® wanaweza kukumbana na madhara mabaya wakati wa kutumia bidhaa. Ikiwa madhara yoyote mabaya yatatokea, matumizi ya bidhaa yanapaswa kukomeshwa mara moja. Dalili za madhara mabaya ya ngozi zinaweza kujumuisha upele, na uvimbe, ambayo kwa kawaida hutokea katika eneo ambalo bidhaa hiyo ilitumika. Madhara haya yanaweza kuambatana na mwasho na usumbufu kidogo. Katika hali nyingi, madhara mabaya yatapungua ndani ya siku mbili hadi tatu baada ya matumizi ya bidhaa hiyo kukomeshwa. Hadi ngozi irudi hali yake ya awali, inaweza kuonekana kavu na iliyo parara madhara yakiendelea kupungua. Ikiwa una wasiwasi wowote kuhusu athari ya mzio inayoweza kutokea kutokana na kutumia Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil®, ni busara kufanya jaribio rahisi la mzio ili kuangalia hii. Hii inafanywa kwa kutumia kiasi kidogo cha bidhaa hii kwenye kigasha cha ndani na kusubiri kwa muda wa saa 24 ili kuona ikiwa athari yoyote itatokea. Uwekundu unaoonekana wa ngozi (harara) au uvimbe mdogo wa ngozi (uvimbe) unaweza kuonyesha uwezekano wa athari ya mzio.

VITU VISABABISHAVYO MIZIO

Kama ilivyo na vitu vingi visababishavyo mizio, hivi vipo katika mafuta ya mimea na manukato. Hivyo ni: Alpha-Isomethyl Ionone, Amyl Cinnamal, Benzyl Salicylate, Citronellol, Coumarin, Eugenol, Farnesol, Geraniol, Hydroxycitronellal, Limonene, na Linalool.

KUMEZA KWA BAHATI MBAYA

Katika tukio la kumeza kwa bahati mbaya Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil®, haiwezekani kwamba athari yoyote mbaya zaidi ya hisia za kichefuchefu na kuhara zitapatikana kwa sababu Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® hayana sumu. Hata hivyo, inashauriwa kutafuta ushauri wa matibabu, hasa katika hali ya mtoto mchanga au mkubwa kumeza kwa bahati mbaya.

KIPINDI CHA BAADA YA KUFUNGUA (PAO)

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yana PAO ya miezi 36. Hii ni kipindi cha muda baada ya kufungua ambacho bidhaa ni salama na inaweza kutumika bila madhara yoyote kwa mtumiaji.

UTENGENEZAJI

Utengenezaji wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® unafuata mahitaji ya Kanuni Bora za Utengenezaji (GMP) ya ISO 22716: 2007 kwa bidhaa za vipodozi. Malighafi zote zinazotumika katika utengenezaji wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® zinaambatana na Cheti cha Uchanganuzi (COA), na vifaa vyote vya ufungaji vinaambatana na Cheti cha Ukubalifu (COC). Hakuna malighafi au vifaa vya ufungaji hutolewa ili kutengenezwa hadi vipite vipimo vya kudhibiti ubora. Kila bechi ya Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® iliyochanganywa imetengewa nambari ya kipekee ya bechi. Sampuli kutoka kwenye bechi hiyo hujaribiwa kwenye maabara ili kuangalia mwonekano, uwazi, harufu, utambulisho kwa kutumia na spectrophotometry, uzito, unato na mikrobiolojia. Sampuli huhifadhiwa kwa miaka sita. Ujazaji na ufungaji wa Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® hufanyika katika kituo kilichodhibitiwa halijoto na unyevu. Hewa hupita kupitia mfumo wa hali ya juu wa kuchuja hewa (HEPA) ili kuzuia uchafuzi wa vumbi. Wafanyakazi wanaofanya kazi kwenye viwanda vya uzalishaji huvaa kofia, barakoa, ngao za uso, glavu, kanzu na vifuniko vya viatu. Sampuli huondolewa viwandani katika vipindi vya mara kwa mara na hukaguliwa na idara ya Udhibiti wa Ubora kama tahadhari dhidi ya kasoro isiyo ya kawaida. Nambari ya bechi huchapishwa kwenye chupa, katoni na shehena, na sampuli ya kubakiza kutoka kwenye kila bechi iliyotengenezwa huhifadhiwa kwa miaka sita.

MAELEKEZO YA UHIFADHI

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yanapaswa kuhifadhiwa mahali baridi, mbali na miali ya moja kwa moja ya jua.

UREJELEZAJI

Bidhaa zote zinazofunga Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® (chupa, kifuniko na katoni) zinaweza kutumiwa tena.

UTHIBITISHO

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yamethibitishwa kuwa Halaal na Kosher.

HAIJAJARIBIWA KWENYE WANYAMA

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® na malighafi zake hutengenezwa viwandani kwa kufuata kanuni za EU zinazohusiana na kuwajaribu wanyama kwa madhumuni ya vipodozi. Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil®, au viungo vyake vyovyote, havijajaribiwa kwenye wanyama na Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil au watoaji wao wowote wa malighafi.

HAINA BIDHAA ZA WANYAMA

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® hayana viungo vyovyote vinavyotokana na wanyama.

MABADILIKO KATIKA MWONEKANO

Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® yana calendula, chamomile, lavender na vitu vilivyotolewa katika mimea ya rosemary na mafuta muhimu, pamoja na vitamini A, ambazo zote zinaathiriwa na mwangaza. Kuwekwa kwenye jua kunaweza kusababisha mabadiliko ya rangi baada ya muda. Hata hivyo, haina uwezekano wa kuathiri ufanisi wa bidhaa. Kama tahadhari, chupa za Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil® zina kifyonzaji cha UV. Hata hivyo bidhaa hii inapaswa kuhifadhiwa mbali na mionzi ya moja kwa moja ya jua.

UFUNGAJI

Picha ya bidhaa ya Mafuta ya Kutunza Ngozi ya Bio‑Oil